KAULI mbalimbali zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa ziara zake zimezua taharuki jijini humo.
Kwa nyakati mbalimbali wakati wa ziara zake, Makonda anadaiwa kutoa kauli za vitisho hasa kwa watumishi wa umma.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha ACT-Wazalendo kimemshtaki mkuu huyo wa mkoa katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Utawala Bora ili imuwajibishe.
Katika taarifa yake iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Katibu wa Ngome ya Wanawake wa chama hicho, Esther Kyamba alisema kauli alizozitoa Makonda zimewadhalilisha watumishi hao.
“Tumesikitishwa na kuhuzunishwa na kauli zisizo za kiuongozi na zisizozingatia kanuni za maadili ya utumishi wa umma zinazoendelea kutolewa na RC Makonda.
“Jana (juzi), katika mkutano anaouita wa kutatua kero kwa wakazi wa Dar es Salaam aliendelea kushindwa kutatua kero na badala yake kuongeza kero ya kudhihaki, kudhalilisha kukejeli na kutukana hadharani wananchi anaowaongoza na watumishi anaowasimamia kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya Watanzania,” alisema.
Kyamba alisema kitendo cha Makonda kumtolea lugha ya udhalilishaji Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni, Rehema Mwinuka akiwa Mabwepande kwa kumtamkia kwamba “Hawa ndio vichaa tunaohangaika nao, toka hapa”. Hakikubaliki.
“Kauli hiyo imetushtua sana,tunalaani kwa nguvu zetu zote, kauli kama hii si tu haikupaswa kutolewa na kiongozi mkubwa katika ngazi ya mkoa lakini pia ni kauli mbaya ambayo ililenga kumdhalilisha Rehema na kumvunjia heshima yake mbele ya umma,” alisisitiza.
Alisema kutokana na udhalilishaji huo uliofanywa na Makonda, wameshawasilisha mashtaka yao dhidi yake mbele ya Tume, wakiitaka imwajibishe kwa kitendo chake hicho cha utovu wa nidhamu na maadili ya utumishi wa umma.
“Ngome inamtaka mkuu huyo wa mkoa kutambua kuwa kwa kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma, kanuni ya 65(1) inamtaka mtumishi wa umma, “kuepuka kufanya vitendo viovu au kutamka maneno yanayolenga kuwaaibisha watumishi wa ngazi moja, za chini yao au wa vyeo vya juu,” alisema.
Alisema kitendo alichofanya, kumwaibisha na kumtolea lugha ya udhalilishaji, Mwinuka ni kinyume cha Sheria na Kanuni za Utendaji katika Utumishi wa Umma.
“Tunaitaka Tume ifanye uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya matamshi mbalimbali yaliyotolewa na Makonda ambayo yalikiuka sheria ya Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.
“Tunayataka mashirika na asasi mbalimbali zinazosimamia haki za binadamu, haki za jinsia na utawala bora kupaza sauti dhidi ya kauli isiyo ya kiuongozi ya Makonda, Ngome na Chama kwa ujumla tutaendelea kuwasemea wanyonge wote popote walipo kwa kadri ya uwezo wetu,” alisema.