Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, imedaiwa kuwataja katika orodha ya wadaiwa sugu watu ambao baadhi yao hawajasoma Tanzania na baadhi yao wakidai kuwa washamaliza kulipa madeni yao na huku wengine wakidai kuwa hawakusoma chuo kikukuu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano, Cosmas Mwaisoba amejibu maswali hayo yaliyokuwa yakiulizwa katika kipindi cha mahojiano cha JAMBO kinachorushwa na TBC1 akiombwa kutoa ufafanuzi baadhi ya watu waliowekwa kwenye orodha ya wadaiwa ambao hawahusiki na madeni hayo, Mkurugenzi huyo alijibu.
“Kuna watu ambao wamesoma nje ya nchi ambao wamekopeshwa sio kwamba kusoma nje ya nchi ndio mtu hukukopa hapana, wapo waliosoma nje ya nchi kwa kupata scolarship za nchi kadhaa ambapo bodi iliwakopesha, sasa kama kuna mtu ambaye alisoma nje ya nchi na alijisomesha mwenyewe hakupata mkopo wa bodi nadhani huyo ndiye ana haki ya kulalamika, sasa yeye atakachotakiwa kukifanya kuwasiliana nasi ili tuweze kuwangalia hiyo kesi yake ikoje akiwa na vielelezo vyake baadaye taarifa zitarekebishwa,”alisema Mwaisoba.
“Kama tumefanya makato kimakosa kwa mtu ambaye hatumkopesha taarifa zinarekebishwa na kwa kiasi cha fedha ambacho amekatwa kitarejeshwa na kuna watu wengine wamelalamika kwamba sikusoma chuo kikuu na nakatwa kwahiyo malalamiko hayo tumeyapokea lakini tukiangalia kwenye kumbukumbu zetu tuliangalia tatizo hili chanzo au tatizo kubwa la suala hili tuligundua ni kwamba taarifa zinakuwa zinamchanganyiko na hasa kufanana kwa majina,”aliongeza.
Bodi ya Mikopo iliwapa siku 30 wadaiwa sugu wa mikopo hiyo kuirejesha.