Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi kufuatia
vifo vya watu 11 vilivyosababishwa na ajali ya basi la kampuni ya
Barcelona iliyotokea jana tarehe 17 Oktoba, 2016 katika eneo la Miteja
Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.
Basi
hilo lenye namba T 101 CUU lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam
kwenda Kijiji cha Mahuta katika Wilaya ya Newala Mkoani Lindi,
lilipinduka baada ya gurudumu lake la kushoto kupasuka na kusababisha
vifo vya watu 10 papo hapo na mwingine 1 kufariki dunia baadaye akiwa
anapatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Lindi, huku watu
wengine 43 wakiwa wamejeruhiwa.
Katika
salamu zake, Rais Magufuli amesema amepokea taarifa za vifo vya watu
hao kwa mshituko na huzuni kwa kuwa kwa mara nyingine Taifa limepoteza
watu wake na familia zimepoteza wapendwa wao na watu ambao ziliwapenda
na kuwategemea.
"Ndugu
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi naomba unifikishie salamu
nyingi za pole kwa wote waliopoteza jamaa na ndugu zao katika ajali hii,
kwa hakika nimeguswa sana na vifo hivi na naungana na familia za
marehemu wote katika maombolezo na sala" amesema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli amewasihi wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa subira
na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi na
amewaombea Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Pia
Rais Magufuli amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili waungane na
familia zao na kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa,
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2016.