WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Lindi kuhakikisha
wanawakamata na kuwachukulia hatua watu wote wanaoharibu mazingira kwa
kufyeka na kuchoma moto misitu kwa sababu wanaharibu mazingira na
kusababisha ukame.
Amesema
mkoa huo upo hatarini kugeuka jangwa na tayari vyanzo vingi vya maji
vimeanza kukauka kwa sababu ya uharibifu wa mazingira unaotokana na watu
kufanya shughuli za kijamii kwenye vyanzo vya maji.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana Jumanne, Oktoba 18, 2016 wakati akizungumza
kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa katika mikutano
iliyofanyika kwenye vijiji vya Nanjaru, Nachinyimba, Nambiranje,
Mkaranga, Nandenje, Nachinyimba na Mandarawe.
Alisema
wakulima wa ufuta wanatakiwa kuendelea kutumia mashamba yao ya zamani
na kuacha tabia ya kufyeka misitu kila mwaka na badala yake waanzishe
mpango wa upandaji miti ili kuepusha taifa kugeuka kuwa jangwa.
“Vyanzo
vya maji vimekauka kwa sababu tumekata miti mingi. Mito yote iliyokuwa
inatiririsha maji imekauka. Viongozi wa mkoa hakikisheni misitu
inalindwa na atakayekutwa analima kwenye vyanzo vya maji akamatwe,”
alisema.
Waziri
mkuu aliongeza kuwa “Ukataji miti huu unaoendelea katika maeneo yetu
hakutosababisha kukosekana kwa maji tu, bali hata mazao yatapungua.
Jambo hili itasababisha njaa katika vijiji vyetu, hivyo tuache kukata
miti.
Waziri
Mkuu alisema kwa sasa Serikari inatumia gharama kubwa kuchimba visima
virefu kutafuta maji. Amesema zamani walikuwa wanachimba mita 20 au 30
wanakuta maji na gharama yake ilikuwa sh. milioni 35, ambako kwa sasa
wanalazimika kuchimba mita zaidi ya 150 kwa gharama y ash milioni 75 kwa
kisima kimoja.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi,aliwataka
watendaji wa kata na vijiji kuimalisha ulinzi wa maeneo ya misitu na
maji, na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hatuko
tayari kutengeneza jangwa hivyo tutapamba na wale wote wenye tabia za
kuchoma moto misitu au kulima kwenye vyanzo vya maji,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMNNE, OKTOBA 18, 2016