OFISA wa kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani Arusha, Wanguluke Shilinde, nusura aende jela miaka sita baada ya kukutwa na makosa mawili ya kushawishi kupewa rushwa pamoja na kupokea rushwa ya Sh milioni tatu kutoka Kampuni ya Lachan Tanzania Ltd.
Ofisa huyo amelipa faini ya Sh milioni moja na kuachiwa huru. Alitakiwa kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kila kosa au kwenda jela, amechagua kulipa faini.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augustino Rwizile akisoma hukumu hiyo leo amesema, mahakama imemtia hatiani Shilinde baada ya kujiridhisha kuwa alikutwa na fedha za rushwa zilizotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akiwa amezificha kwenye soksi.
Amesema, mshitakiwa huyo aliomba rushwa kwa mtumishi wa kampuni hiyo, Lucy Magufa ili amfanyie makadirio ya kodi ya kampuni yake, ambayo alidai alitakiwa kulipa Sh milioni 75, lakini akadai ana uwezo wa kupunguza fedha hizo hadi Sh milioni tatu.