Wabunge wameibana Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) kwa kuongeza posho na kufikia jumla ya Sh1 bilioni katika kipindi kifupi kiasi ambacho hakilingani na kazi wanayoifanya.
Kwa kipindi kirefu, bodi hiyo imekuwa ikitupiwa lawama kwa kuchelewesha mikopo, kushindwa kukusanya fedha za wanafunzi waliokopa na kutoa mikopo kwa wanafunzi hewa.
Hivi karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema bodi hiyo imetoa fedha za kujikimu na mafunzo kwa vitendo kwa zaidi ya wanafunzi hewa 1,000.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Abdul-Razaq Badru alijitetea mbele ya kamati hiyo akisema ni mgeni katika bodi hiyo na kwamba wanaweka mikakati mizuri ya kurekebisha mambo hayo ili kuhakikisha inafanya kazi kwa weledi zaidi.
Wakizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) cha kukagua Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2014/15 ya bodi hiyo, wabunge hao walisikitishwa na kitendo cha bodi hiyo kushindwa kukusanya zaidi ya Sh3 trilioni walizowakopesha wanafunzi mbalimbali tangu ianze kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Walisema isipobadilika katika utendaji wake, kuna haja ya Serikali kuivunja na kuchagua benki moja kusimamia shughuli hiyo.
“Mnatakiwa kuongeza juhudi na mikakati ili kuhakikisha kwamba madeni yote yanakusanywa kwa wakati la sivyo naona kuna haja ya Serikali kuivunja bodi nakutafuta njia nyingine,” alisema Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Raisa Mussa.
Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka alihoji kwa nini pamoja na bodi hiyo kuwa na mameneja 18 na wafanyakazi wa kudumu 144, bado utendaji wao umekuwa siyo wakuridhisha.
“Kwa idadi yenu tulitegemea kupata ripoti inayojitosheleza na hata utendaji wenu ulitakiwa kuwa wa ufanisi zaidi,” alisema.
Akijitetea zaidi, Badru alisema kuna changamoto nyingi zinazoikabili bodi yake lakini kwa sasa wamepiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wanufaika wa mfuko huo.
“Kwa mfano Mei mwaka huu tulikusanya kiasi cha Sh2 bilioni na Juni tulikusanya Sh6 bilioni,” alisema.
Aliongeza kuwa ipo mikakati mingi ambayo wamejiwekea katika kuhakikisha kwamba bodi hiyo inakusanya madeni kikamilifu kutoka kwa wadeni wake wote.
“Kwa kupitia mikakati yetu, tumeweza kuongeza idadi ya wanafunzi ambao tunawapa mikopo kutoka 42,729 hadi 123,783. Katika kipindi hicho fedha za mikopo zimeongezeka kutoka Sh56 bilioni hadi kufikia Sh465.3 bilioni,” alisema.