VIONGOZI
wa vyama vya siasa wanaounda Klabu ya Viongozi wamesema hawaungi mkono
maandamano yaliyopangwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
katika kulinda amani ya nchi.
Mwenyekiti
wa klabu hiyo, Fahmi Dovutwa alisema uamuzi wa kutounga maandamano hayo
imefikiwa kwenye kikao cha viongozi wa vyama wa siasa wa klabu hiyo
waliokutana jana kujadili hali ya siasa nchini.
“Vyama
vya siasa tumekutana leo (jana) ili kufanya tafakari juu ya hali ya
siasa nchini hususan tamko la Chadema la kufanya maandamano na hatimaye
mikutano sehemu mbalimbali. Pia tumezingatia tamko lililotolewa na
Serikali na Rais John Magufuli la kutaka amani ya nchi idumishwe, hivyo
hatuungi mkono maandamano,” alisema.
Alisema
pamoja na kutounga mkono, viongozi hao wanataka kufanyika kwa mkutano
ambao utashirikisha vyama vyote vya siasa nchini ili kupata muafaka
ambao utaepusha nchi kuingia katika malumbano na misuguano.
“Tarehe
waliyopanga kufanya hayo maandamano ni maadhimisho ya Siku ya Majeshi
Duniani kote, hivyo wanajeshi watakuwa na shughuli zao ambazo zinaweza
kuleta taswira ya jeshi kuingilia maandamano, lakini jambo la msingi ni
kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa vyama vyote,” alisema Dovutwa.
Vyama
vilivyohudhuria mkutano huo ni Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Alliance
For Tanzania Farmers Party (AFP), Chama cha Democratic (DP), D-Makini,
JAHAZI Asilia, Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), United
Peoples Democratic Party (UPDP), ADA-TADEA na Chama Cha Kijamii (CCK).
Hivi
karibuni, Chadema ilitoa tamko la kufanya maandamano na mikutano nchi
nzima katika kampeni waliyoiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania
(UKUTA).
Azma
ya Chadema inakuja baada ya siku kadhaa za Jeshi la Polisi kuzuia
mikutano ya hadhara na maandamano kwa sababu za kiusalama.
Hata
hivyo, Rais Magufuli alipiga marufuku maandamano hayo kwa lengo la
kutaka amani ya nchi idumishwe na kuelekeza mikutano ya hadhara ya
wabunge walioshinda ifanywe kwenye majimbo yao.