Serikali
imewatoa hofu wananchi kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao inayoanza
kutumika rasmi leo kuwa haijatungwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, bali kwa maslahi mapana ya
taifa na kuleta maendeleo ya nchi, kujenga uchumi imara na kupambana na
wahalifu.
Aidha,
serikali imewasisitizia wananchi kutumia vizuri mitandao kwa faida yao
na taifa na kujiepusha na mambo ambayo yanakatazwa na sheria hiyo ili
kutoingia matatani.
Hayo
yalisemwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame
Mbarawa, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana kuhusu kuanza rasmi kutumika kwa sheria hiyo na ya miamala ya
kielektroniki.
“Serikali
imejiridhisha baada ya kufanya maandalizi yote muhimu ikiwamo kutoa
elimu kwa umma na kujenga uelewa kwa watekeleza wa sheria hizi. Sasa
sheria hizi zitaanza kutumika rasmi Septemba 1 (leo),” alisema Prof. Mbarawa.
Alisema
sheria hiyo itasaidia kupambana na uhalifu kwenye mtandao kutokana na
watu wengi kutumia vibaya mtandao na kuwalaghai watu kutuma fedha ama
kuiba katika mabenki.
Alisema
kwa mujibu wa sheria hiyo, watu wanaosambaza meseji za uchochezi ama za
uongo kwa watu wengine ni kosa la kisheria na kufanya hivyo watakumbana
na adhabu kali.
Alisema mtumiwaji wa meseji za aina hiyo akifuta pasipo kusambaza kwa watu wengine sheria hiyo haitamwadhibu wala kumhusu.
“Sehemu
ya kifungu cha sheria ya makosa ya mtandao, kifungu cha 16 kinaeleza:
mtu atakayechapisha taarifa au data katika picha, maandishi, alama
au katika namna nyingine yoyote katika mfumo wa kompyuta, huku akijua
kwamba taarifa au data hizo ni za uongo, zinapotosha, zisizo sahihi, na
kwa lengo la kudhalilisha, kutishia, kuudhi au kwa njia nyingine au
kudanganya umma au kuchochea utendaji wa kosa, atakuwa ametenda kosa na
akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh. milioni tano au
kutumika kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja,” alisema.
Prof.
Mbarawa alitoa wito kwa wananchi wazingatie matumizi salama na sahihi
ya huduma za mawasiliano na mitandao kwa manufaa ya kila mtu na kwa
maendeleo ya taifa na kuepuka matumizi yasiyo sahihi.
Baadhi ya makosa ambayo yanaweza kukufanya ushtakiwe
- Kuweka mtandaoni picha za kingono za watoto
- Kuweka mtandaoni picha za ngono au za utupu
- Kuweka taarifa za uongo mtandaoni
- Kuweka taarifa za uchochezi mtandaoni
- Kutukana au kumdhalilisha mtu
- Kuweka mtandaoni tetesi zisizothibitishwa
- Kutukana au kumdhalilisha mtu kwa misingi ya udini/ukabila.
0 comments:
Chapisha Maoni