Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe ameachiwa saa saba na robo usiku wa kuamkia leo baada ya kuhojiwa
na kupekuliwa na Jeshi la Polisi.
Mbowe alikamatwa jana Jumatatu jioni wakati
akienda kujisalimisha polisi na kupekuliwa nyumbani kwake kabla ya
kuhojiwa hadi alipoachiwa usiku wa manane.
Ofisa habari wa chama hicho,
Tumaini Makene amethibitisha taarifa za kuachiwa
mwanasiasa huyo kuwa ni za kweli.
Hata hivyo, taarifa
iliyosambazwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu kupitia
mitandao ya kijamii imesema kuwa chama hicho kitatoa taarifa zaidi juu
ya tukio hilo leo.
“Tunawashukuru wote kwa sala, maombi na subira
na hivyo kuhitimisha salama saa kumi za mwenyekiti wetu kuwa chini ya
Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam,” Mwalimu
amesema.