Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameitaka Mamlaka ya
Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kusitisha bei mpya ya umeme
iliyotangazwa juzi na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlamgosi.
Taarifa ya kusitisha kwa bei hiyo ilitolewa jana na Profesa Muhongo kupitia barua yake kwa Ewura.
Muhongo
amesema kuwa amesitisha bei hiyo mpya kwa sababu nne, ikiwamo
kutoshirikishwa katika mchakato huo akiwa ni waziri mwenye dhamana.
“Ewura
walipokwenda mikoani Watanzania wote walipinga bei kupanda, wao
wametumia kigezo kipi cha kupandisha? Pili taratibu zilizopo ni kwamba
Tanesco wanapeleka maombi Ewura, kisha Ewura wanafanya zoezi hilo la
kuuliza wahusika watumiaji wa umeme, baada ya hapo wanatengeneza ripoti
wanaileta wizarani, na ningaliipata hiyo ripoti.
“Hivi
tunavyoongea sijaipata mkononi, nikiipata nitaiita Ewura na Tanesco
tunajadili na baada ya hapo ndipo wanaenda kutangaza. Wao wametangaza
hata mimi taarifa nazipata kama wewe,” alisema Profesa Muhongo.
Katika
sababu ya tatu ya kusitisha bei hiyo, Profesa Muhongo alisema hakuna
ukweli kuwa kupandisha bei ya umeme kutasababisha Tanesco imalize
matatizo yake kifedha.
“Tanesco
kila mwaka inapandisha bei, mbona hawajajikwamua? Mbona madeni yanazidi
kuongezeka? Nyingine ni kwamba tunakopa fedha kutoka nje ya nchi na
watakaolipa hilo deni ni Watanzania wote, sasa hatuwezi kukopa kulipa
madeni ya Tanesco halafu shukrani tutakayoipata ni kupandishiwa bei ya
umeme tena.
“Nyingine
nenda ufuatilie Tanesco wana matumizi mabaya ya fedha, nimesitisha
zoezi lao, sijui kama hizo fedha wamerudisha, unajua wanapeana wale
walioko juu bonasi kati ya Sh milioni 40 na milioni 60 kwa mwaka,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema
Ewura wanapaswa kupeleka ripoti ijadiliwe, kwani haiwezi kuwa Serikali
ndani ya Serikali na haiwezi kupandisha bei bila waziri mwenye dhamana
kujua kwa kuwa inapata bajeti kutoka bungeni.