Mabadiliko
yaliyofanywa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekuja na mkakati
mpya wa kuwavua ‘gamba’ makada wa chama hicho wenye ukwasi waliovuna
kinyume na taratibu.
Katibu
wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey
Polepole amesema kuwa wako katika mkakati wa kukisafisha zaidi chama
hicho, akiwataka matajiri wenye ‘makandokando’ wajiondoe mapema.
“Kuwa
tajiri si dhambi na si kwamba CCM inafukuza matajiri, hapana. Tatizo
letu kama CCM katika mwelekeo mpya, mtazamo mpya na maegeuzi
yanayofanyika, hatuhitaji kuwa na aina ya matariji wanaojipatia utajiri
wao kwa hila, kwa rushwa na kwa dhuluma,” alisema Polepole katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini.
“Ukijiona
wewe ni tajiri na mikono yako ni michafu kwa maana ya kuwa na makando
ya kukosa uaminifu, hulipi kodi, ukae mbali na CCM,” aliongeza.
Alisema
watawachukulia hatua za kuwaondoa ndani ya chama hicho na kuwakabidhi
kwa vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Tangu alipochaguliwa, Polepole amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho kitajikita katika msingi wake wa kuwatumikia wanyonge.
Mkakati
huo wa kuwang’oa matajiri wasiowaaminifu ndani ya chama hicho unafanana
na oparesheni iliyobatizwa jina la ‘Vua Gamba’ ndani ya chama hicho
miaka kadhaa iliyopita, iliyolenga kuwang’oa viongozi na vigogo ambao
walibainishwa kujipatia mali kinyume cha utaratibu na mafisadi.