Sheria ya kuwalinda watoa taarifa na mashahidi wa kesi za uhalifu imeanza kutumika rasmi na kwamba itarahisisha upatikanaji wa taarifa hizo kwakuwa watakao vujisha siri za watoa taarifa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mnamo tarehe 25 Machi Mwaka huu, sheria hiyo ilitangazwa katika gazeti la serikali kupitia tangazo namba 110 na kuidhinishwa kwa ajili ya matumizi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe Julai 1,2016.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Utekelezaji wa Katiba wa Wizara ya Katiba na Sheria Kamana Stanley, amesema kuwa sheria hiyo pia itashughulikia wanaotoa taarifa za watoa siri kwa wanaotuhumiwa na kwamba mtoa taarifa akipata madhara, aliyehusika kutoa taarifa hizo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Kuwepo kwa sheria hii kutasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wanaotoa taarifa za za uhalifu wa makosa ya aina mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka, ” amesema.
Ameongeza kuwa ” Aidha, kwa wale watakaoshindwa kushughulikia vyema taarifa zinazotolewa kwao na kuruhusu watoa taarifa na watoa ushahidi kupata madhara, sheria imeweka utaratibu wa namna ya kushughulika nao. “
Stanley amesema kuwa, licha ya wavujisha siri za watoa taarifa kuchukuliwa hatua za kisheria, pia watoa siri wanaopata madhara kwa sababu ya kutoa taarifa hizo watapewa fidia.
“Inatarajiwa kwamba kutungwa kwa sheria hii kutaleta matokeo chanya katika kupambana na uhalifu wa aina zote nchini, ” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu ili kuisadia serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu.

