Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakifurahia ngoma ya asili ya
kabila la Wafipa wakati walipowasili kwenye kijiji cha Mtowisa mkoani
Rukwa kuzungumza na wanachi Agosti 24, 2016.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa
inatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia mwezi ujao
baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliokuwa unajengwa.
Mradi
huo unajengwa kwa usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira, Manispaa ya Sumbawanga (SUWASA), kwa ufadhili wa nchi za
Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani kupitia benki yake ya
Maendeleo (KfW), sh. bilioni 31 utakapokamilika.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati na
akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji safi na usafi wa mazingira
katika Manispaa ya Sumbawanga na kuitaka kampuni ya kampuni ya Techno
Fab Gammon Joint Venture ya India kumaliza ujenzi wa mradi huo haraka
iwezekanavyo.
Amesema
mradi huo ambao tayari umekamilika kwa asilimia 85 unatarajiwa
kukamilika Septemba mwaka huu, hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha
wanashirikiana na Manispaa katika kulinda miundombinu ya mradi huo mara
utakapokamilika pamoja na kutunza vyanzo vya maji.
“Pamoja
na Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji
inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini,changamoto ya upatikanaji
wa huduma hiyo imekuwa kubwa kutokana na baadhi ya visima vimeanza
kukauka hali inayosababishwa na uharibifu wa mazingira,” amesema.
Amesema
kumekuwa na uvamizi mkubwa katika maeneo ya vyanzo vya maji ambapo
wananchi wanajishughulisha na shughuli za ulimaji, uchungaji wa mifugo,
ujenzi wa nyumba za makazi na uchomaji misitu hivyo kusababisha uchafuzi
wa mazingira na hatimaye vyanzo hivyo hukauka.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wote wa wilaya na wenyeviti wa
vijiji nchini kuyasimamia maeneo yenye vyanzo vya maji na kuwaondoa watu
wotewalioyavamia kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na
kuwafikisha mahakamani.
Naye
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye
alimuwakilisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge
katika hafla hiyo alisema aliishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa
nchi za Ulaya kwa kufadhili mradi huo.
Hata
hivyo Mhandisi Kamwelwe alisema suala la kuhifadhi mazingira ni msingi
endelevu wa upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo aliwaomba wananchi
kujiepusha na uchafuzi wa vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira ili
kuepuka athari ya Taifa kukubwa na janga la ukame.
“Wananchi
wanatakiwa kuacha kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kulima, kufuga
ndani ya mita 60 kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji
ili kuepusha uharibifu wa mazingira ambao madhara yake ni makubwa kwa
viumbe wote,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, AGOSTI 25, 2016.