Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa shughuli ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM haikuwa rahisi na akashukuru kwamba imemalizika kwa amani.
Mchakato
huo ulihitimishwa Julai 12 mjini Dodoma wakati Mkutano Mkuu wa CCM
ulipopitisha jina la Dk John Magufuli kugombea nafasi ya kuongoza
Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda
wake mwishoni mwa mwaka.
Jumla ya makada 38
walijitokeza kuwania nafasi hiyo, na majina matano ndiyo yaliyopitishwa
kwenda Halmashauri Kuu na baadaye matatu kwenda Mkutano Mkuu.
Mchakato
wa urais ndani ya CCM ambao kwa kawaida hutawaliwa na msuguano kabla ya
kumalizika kwa maridhiano, safari hii ulienda mbali zaidi baada ya
wajumbe watatu wa Kamati Kuu kupinga nje ya kikao uamuzi wa chombo hicho
na baadaye wajumbe wa Halmashauri Kuu kumwimbia mwenyekiti wao, Jakaya
Kikwete wimbo wa kuonyesha wana imani na Edward Lowassa baada ya jina la
mbunge huyo wa Monduli kuenguliwa na Kamati Kuu.
Jana,
akitoa hotuba fupi baada ya kumalizika kwa sala ya Eid el Fitr kwenye
viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mwinyi alizungumza kwa
mara ya kwanza hadharani kuhusu mchakato huo, akidokeza hali ilivyokuwa.
“Haikuwa
kazi rahisi kwenye mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye
peperusha bendera ya CCM,” alisema Mwinyi lakini akawahi kuipoza kauli
hiyo kwa kuelezea amani ilivyotawala mwishoni.
“Kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.”
“Uchaguzi
huu ni kwa ajili ya kuwapata viongozi wetu, tunataka viongozi bora wa
kutuletea maendeleo, mapatano na wenye mahaba na wananchi.”
Akizungumza
hadharani kwa mara ya kwanza baada ya mchakato huo wa kumtafuta mgombea
wa urais kukamilika mjini Dodoma, Mzee Mwinyi alimshukuru Mungu kwa
mchakato huo kuisha salama.
“Haikuwa kazi rahisi kwenye
mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye peperusha bendera ya
CCM, kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.
“Sasa,
ninawaomba Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi wa
nchi tunaoufanyika kila baada ya miaka mitano,“ alisema Rais Mwinyi
ambaye alikuwa mmoja ya wajumbe wa Baraza la Ushauri waliofanya kazi ya
kutuliza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM hadi kuafikiana kuendelea na
mchakato wa kumpata mgombea urais.
Aliwasisitizia
Watanzania kuacha tabia ya kupenda mno na kuacha kubaguana, akisema
hakuna aliye bora na kuwataka kuzidisha mapenzi miongoni mwao na
kusherehekea vyema Sikukuu ya Eid el Fitr.
“Hakuna jambo lenye maana kama hili la kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kutufikisha salama siku kama hii ya leo (jana) ambayo tunasherekea Sikukuu ya Eid,” alisema Mwinyi.
“Hakuna jambo lenye maana kama hili la kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kutufikisha salama siku kama hii ya leo (jana) ambayo tunasherekea Sikukuu ya Eid,” alisema Mwinyi.
Awali Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad
Mussa Salum aliwasisitizia wananchi umuhimu wa kusherekea sikukuu hiyo
katika hali ya amani na utulivu.
Pia, aliwashauri
wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao sehemu zenye maadili ili
washerehekee kama ambavyo Mwenyezi Mungu anapenda.
“Leo
(jana) ni siku ya furaha, naomba tusherekee maeneo salama pia Waislamu
msisahau kufunga sita kwani ina malipo makubwa,” alisema Alhad Salum.
Mkoani
Geita ambako ilifanyika sala ya kitaifa ya Eid, Makamu wa Rais, Dk
Mohamed Gharib Bilal alihutubia Baraza la Eid na kusema kipindi hiki
kinahitaji utulivu, kuelewa na kuheshimiana pamoja na kudumisha uhusiano
ili Taifa lipate viongozi bora.
“Tuwe watulivu ili
Tanzania ibaki kuwa nchi ya kukimbiliwa na isiwe nchi ya kukimbiwa...
sisi tusiwe wakimbizi, tuwe watu wa kupendana, kuvumiliana na
kuthaminiana. Tusifikie hatua ya kuchukiana, kuuana na kufanyiana
ukatili,” alisema Dk Bilal.
Alisema amani inaweza
kuvunjwa na mtu yoyote kwa namna yoyote ile, akaharibu mazuri na heshima
ya Taifa na akawaomba wananchi na waumini wote wasifikie hatua hiyo
akisema ndiyo wenye uwezo wa kuifanya nchi yao kuwa ya amani.
“Tuishi
kwa kuheshimiana, kupendana na kuvumiliana tushikamane katika, hali
iliyopo sasa kwa nchi yetu siyo nzuri. Si ajabu hivi sasa tunavyoongea
kuna sehemu mabomu yametokea, si ajabu kuna watu wameuawa kikatili. Hii
yote ni sababu watu sasa wanapoteza misingi ya kuheshimiana, upendo na
kuvumiliana,” alisema Bilal kwenye Viwanja vya Karangara.
Awali
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania, Bakwata, Sheikh Suleiman
Lolela alisema waumini na wananchi wote waitumie vyema nafasi ya
Uchaguzi Mkuu kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaoendeleza
amani.
Kisiwani Unguja, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed
Shein amewataka viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kijamii na
madhehebu ya dini kulinda na kuheshimu msingi na malengo ya kuanzishwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akiuhutubia kwenye
Baraza la Eid el Fitr lililofanyika Ukumbi wa Bwawani na kuhudhuriwa pia
na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad jana, Dk Shein
alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kufanya siasa kwa kuzingatia
misingi ya Katiba na sheria kwa madhumuni ya kuendeleza na kulinda amani
na umoja wa kitaifa kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
“Tunaweza
kushindana bila ya kulaumiana, kukejeliana na tunaweza kushindana bila
ya kudharauliana au kuhasimiana,” alisema Dk Shein kwenye shughuli hiyo
iliyotaliwa na hali ya utulivu.
Alieleza kuwa vyama vya
siasa vimeanzishwa na vipo kwa ajili ya kushindana kwa sera kwa
madhumuni ya kuchochea maendeleo ya Zanzibar na siyo kugombanisha watu
na kuvuruga misingi ya amani na umoja wa kitaifa.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, sheikh wa mkoa, Ahmed Zuber aliwataka Watanzania kudumisha amani na umoja.
Zuber
alisema dunia sasa imechafuka kutokana na uvunjifu wa amani
unaochochewa na siasa chafu hivyo Watanzania bila kujali dini wala
itikadi zao wanapaswa kuilinda amani iliyopo sasa.
“Tunahitaji
utulivu. Nchi nyingi huharibikiwa kipindi kama hiki cha uchaguzi, amani
hupotea kipindi hiki cha uchaguzi. Ndugu zangu Waislamu na msio
Waislamu tukiichezea amani hii iliyopo sasa, tujue hakika hatuna kwa
kukimbilia,” alisema.Mkoani Tanga, imamu wa Msikiti wa Ibadhi, Sheikh
Mohammed Said aliitaka jamii kudumisha amani na utulivu uliopo na kuacha
kushabikia vyama vya siasa.
Sheikh huyo alisema ni
wajibu wa kila mtu kutambua kuwa amani iliyopo ikitoweka ni vigumu
kuirejesha na hivyo kila mmoja ahakikishe anatambua wajibu wake.
Alisema
wakati wa uchaguzi, hutokea jamii kuhamasishana kwa mambo ya kisiasa,
jambo ambalo alisema ni baya na halifai kutokea na hivyo kutaka kila
mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake.Mkoani Lindi, Sheikh Salimu Nalinga akitoa
salamu za Eid el Fitr aliwataka Waislamu kuchagua viongozi waadilifu
ili kuifanya nchi kuendelea kuwa ya amani na utulivu.
0 comments:
Chapisha Maoni